KILIMO MJINI NI HABARI YA MJINI
Na Joina Nzali- Nanenane Morogoro
Afisa kilimo Mfawidhi Manispaa ya Ubungo Editha Chilongani amewasisitiza wananchi hasa wa maeneo ya mijini kutumia kilimo mjini kujipatia chakula na kuokoa fedha ambazo wangetumia kununua mbogamboga kila siku
Chilongani amesema kauli hiyo kwenye maonesho ya Wakulima wafugaji na wavuvi (Nanenane) yaliyoanza tangu Agosti Mosi, na kusema kuwa mtu anaweza kulima katika eneo lake dogo kwa kutumia magunia, makopo au chombo chochote kinachotunza udongo na akazalisha mazao kwa wingi.
"Kwa sasa miji yetu inaongezeko kubwa la watu na ardhi iliyopo ni kwa makazi hivyo kilimo mjini ndio mkombozi kwa ni mtu anaweza akapanda mbogamboga hata kama anaishi ghorofani ukizingatia mbogamboga ni chanzo kikubwa cha madini na vitamini nyingi mwilini" alisema Chilongani
Katika maonesho haya Manispaa ya Ubungo inatoa elimu ya namna ya kulima kilimo mjini, aidha maafisa Ugani wana wajibu wa kuelimisha wananchi kwenye maeneo yao kulima kilimo hiki ili kuwa na uhakika wa chakula katika familia.
Kilimo Mjini kinatafsiri kwa vitendo Kauli mbiu ya maonesho ya Nanenane 2923 "Vijana na wanawake ni msingi imara wa mfumo endelevu wa chakula" ambapo pamoja na kuwa Gorofani mtu anaweza kulima mbogamboga kwa kutumia vifaa rafiki kwa mazingira yake kama vile ndoo, beseni, magunia.