Muhtasari wa Mpango Mkakati wa Miaka 5 ya Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki
Utangulizi
Mkakati huu umeandaliwa kwa lengo la kuboresha Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki. Baada ya kufanyika kwa uchambuzi wa Uwezo, Uzoefu, Fursa na Vikwazo, Mpango Mkakati huu umebainisha maeneo makuu kumi (10) ya kimkakati (stratergic areas) yamebainishwa. Maeneo hayo ni pamoja na: Mapato; Mabadiliko ya Tabianchi; Miundombinu; Usafi wa Mazingira na Afya; Ulinzi na Usalama; Elimu kwa Jamii; Burudani; Habari na Mawasiliano; Utawala na; Usimamizi na Ufuatiliaji. Vilevile, Mkakati umebainisha Dira, Dhamira na Maadili ya kuzingatia katika utekelezaji wake.
DIRA
Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki kuwa kitovu/hazina cha/ya ujuzi/teknolojia ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Ujasiriamali nchini
DHAMIRA
Kuwawezesha wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali kufikia adhma yao kwa: kuimarisha ushirikiano katika uandaaji, utekelezaji na usimamizi wa mipango ya maendeleo ya uwanja; kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma; kuruhusu mawazo mbadala na ubunifu; kuongeza na kudhibiti vyanzo vya mapato; kuimarisha ulinzi na usalama na kuboresha utoaji huduma.
MAADILI
Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki yanazingatia msingi mikuu minane (8) ambayo ni: Ushirikishwaji wa wadau; Ubunifu na Uthubutu; Utendaji kazi uliotukuka; uwajibikaji wa pamoja na uwazi; Haki na Usawa na; mwiko wa kutoa wala kupokea rushwa.
Malengo ya Mpango Mkakati.
Mpango huu umebainisha jumla ya malengo makuu 11 ambayo ni;
- Ukusanyaji wa Mapato unaongezeka na Usimamizi wa matumizi ya Mapato unaboreshwa hadi kufikia mwaka 2025.
- Wadau wa Maonesho wanatambua, kuandaa na kutekeleza mbinu za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika Sekta zao hadi kufikia mwaka 2025.
- Miundombinu ya uwanja wa Nane Nane Kanda ya Mashariki inaboreshwa hadi kufikia mwaka 2025.
- Viwanja vya Nane Nane vinakuwa na mazingira safi na ya kiafya.
- Usalama wa Mali na Miundombinu ya Uwanja unaimarishwa.
- Elimu endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inatolewa kwa jamii.
- Viwanja vya Nane Nane kuwa Kitovu cha Burdani ndani ya Manispaa ya Morogoro.
- Utendaji kazi wa Ofisi ya Meneja wa Nane Nane Kanda ya Mashariki unaimarishwa.
- Usimamizi na Ufuatiliaji wa shughuli za Nane Nane unaimarishwa.
- Washiriki wa Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki wanapewa Motisha ya ushiriki
Usuri wa Mafanikio ya Maonesho ya Nane Nane kwa Sekretarieti za Mikoa
Mpango Mkakati umeonesha mafanikio ambayo Sekretarieri za Mikoa ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga zimeyafikia katika Maboresho ya Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki tangu yalipokabidhiwa rasmi mwaka 2017. Baadhi ya mafanikio hayo ni pamoja na kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato, ujenzi wa ukuta, ukarabati wa miundombinu ya uwanja, Uanzishwaji wa Ofisi ya Meneja na uandaaji wa mpango mkakati wenyewe.
MIKAKATI YA KUBORESHA MAONESHO YA NANE NANE KANDA YA MASHARIKI
Uandaaji wa Tovuti ya Nane Nane na kituo cha Redio
Lengo kuu la mkakati huu ni kuhakikisha kuwa, wadau wa maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki wanapata jukwaa la kutoa maoni, ushauri na kupata habari, taarifa, elimu na burudani wakati wote na mahala popote walipo. Hivyo, uanzishwaji wa kituo vya Redio na Tovuti ya Maonesho ya Nane Nane vitasaidia kufikia adhma hii kwa haraka zaidi.
Uandaaji wa Masterplan ya Uwanja
Pendekezo hili linatokana na changamoto ya ujenzi holela katika uwanja wa maonesho jambo linalozorotesha kuchukua hatua za uboreshaji wa uwanja wa maonesho. Ili kuondoa changamoto hiyo, inapendekezwa kuandaliwa kwa masterplan ya uwanja itakayoonesha layout ya uwanja na wapi huduma gani itawekwa.
Ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
Mkakati huu unazingatia Sera ya Serikali ya awamu ya Tano ya Viwanda na kwakuwa, Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki yanahusika na shughuli za Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ujenzi wa viwanda vidogo vya kusindika bidhaa za Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika uwanja wa maonesho hauepukiki. Hii itahakikisha kuwa, wananchi wanapata fursa ya kuona kwa vitendo hatua za uchakataji wa mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Uwekezaji wa maduka makubwa (Shopping Malls)
Lengo kuu la hatua hii ni kuhakikisha kuwa, Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki yanakuwa active kwa mwaka mzima. Hivyo, uanzishwaji wa maduka makubwa (shopping malls) yatawavutia wananchi kufika katika uwanja wa maonesho mwaka mzima na hivyo kupata fursa ya kuona shughuli za maonesho muda wote.
Uwekezaji katika Nyanja za burudani
Pia, hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa, Uwanja wa Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki unakuwa kitovu cha mafunzo ya kilimo, mifugo na uvuvi na kutoa burudani. Hivyo, uanzishwaji wa huduma za kuogelea, kucheza na kupumzikia utawavutia wananchi kufika katika uwanja wa maonesho kwa mwaka mzima na hivyo kupata fursa ya kuona shughuli za maonesho. Hatua hii pia itasaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Ukarabati na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami nyepesi.
Kwa miaka mingi, maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki yamekuwa yakikabiliwa na changamoto ya vumbi. Hali hii imekuwa ikileta kero na kuathiri afya za washiriki. Pamoja na juhudi mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa ili kupunguza vumbi (kama vile kumwagilia maji na matumizi ya Molases/Makinikia), tatizo la vumbi limeendelea kuwa sugu. Hivyo, hatua hii inalenga kumaliza kabisa changamoto hii.
Ujenzi wa kituo cha kutolea huduma ya kwanza (Kituo cha Afya).
Ukosefu wa huduma ya kwanza katika uwanja wa maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki umewanyima washiriki haki ya kupata huduma ya kwanza mara wapatapo changamoto za kiafya. Hivyo, ujenzi wa kituo cha kutolea huduma ya kwanza utasaidia kuhakikisha kuwa, washiriki wa maonesho wanakuwa na uhakika wa kupata huduma ya kiafya wawapo uwanjani.
Ujenzi wa kituo cha Zimamoto na Uokoaji.
Wakati wa maonesho ya Nane Nane, kuna uwezekano wa kutokea majanga mbalimbali. Hivyo, uwepo wa huduma ya zimamoto na Uokoaji itasaidia kufanikisha kwa haraka shughuli za uokoaji.
Ujenzi na utoaji wa huduma za Malazi (Hostel & Catering).
Wadau wa maonesho wamekuwa wakipata changamoto ya upatikanaji wa huduma za malazi ndani ya maonesho na hivyo kutafuta huduma hiyo nje. Hali hii imekuwa ikiwapunguzia muda wa kusimamia shughuli zao. Hivyo, ujenzi na utoaji wa huduma ya malazi ndani ya uwanja utawaondolea wadau kero hii. Pia, itakuwa chanzo cha mapato ya Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki.
Uanzishwaji wa duka la Shajala (Stationaries).
Kwa muda mrefu, maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki yamekuwa yakikabiliwa na changamoto ya udhibiti wa wananchi na magari yanayoingia uwanjani. Mojawapo ya sababu zinazochangia tatizo hili ni ukosefu wa mfumo thabiti ya kudhibiti matumizi ya vitambulisho na sticker za magari. Hii inatokana na vitambulisho kutowekwa picha za wahusika na stiker kutoandikwa namba za usajili za vyombo husika. Hivyo, uanziswaji wa huduma ya shajala (stationaries) katika Ofisi za Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki utasaidia kutatua changamoto hii. Ofisi ya Meneja itakuwa na vitendeakazi muhimu na hivyo kuwezesha vitambulisho kuwekwa picha za washiriki na stiker za vyombo vya usafiri kuwekwa namba za usajili za vyombo husika. Hii itaondoa changamoto ya matumizi holela ya vitambulisho na pia kuboresha ukusanyaji wa mapato.
Uboreshaji wa eneo la Jukwaa Kuu.
Jukwaa kuu ni sehemu muhimu ambapo wageni rasmi hupatumia kwa ajili ya shughuli za kuzindua na kuhitimisha Maonesho ya sherehe za Nane Nane Kanda ya Mashariki. Hata hivyo, mazingira ya eneo la jukwaa kuu si ya kuridhisha. Hii inatokana na uchakavu wa jengo la jukwaa kuu, ukosefu wa huduma ya choo kwa wageni rasmi na udhaifu wa miundombinu ya umeme. Mapungufu haya yamekuwa yakileta usumbufu na kero kwa wageni na washiriki wakati wa maonesho. Hivyo, mkakati huu unalenga kuboresha madhari ya eneo la jukwaa kuu kwa kujenga jukwaa la kisasa, kujenga choo cha wageni waalikwa na upendezeshaji wa eneo lote la jukwaa kuu.
Uboreshaji wa eneo la Mamalishe.
Kwa muda mrefu, eneo la Mamalishe limekuwa likikabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo ukosefu wa miundombinu ya umeme pamoja na mabanda yenye hadhi kwa ajili ya kutolea huduma za vyakula. Hali hii imesababisha Mamalishe kutengeneza mabanda yasiyokidhi viwango na hivyo kuhatarisha usalama wa walaji na kuchafua mazingira. Hivyo, mkakati huu unalenga kujenga vibanda vya Kudumu eneo la Mamalishe na kuviunganishia huduma za umeme na maji. Hii itasaidia kuongeza hadhi ya eneo hilo, kupunguza uwezekano wa kusababisha magonjwa na kuongeza kipato.
Ujenzi wa vizimba vya kudumu kwa ajili ya washiriki.
Kumekuwepo na changamoto ya udalali wa viwanja na hivyo kuleta usumbufu mkubwa kwa washiriki na kusababisha upotevu wa mapato. Hii inatokana na maeneo mengi ambayo hupimwa vizimba kutokuwa na miundombinu ya kudumu na kutotambulika rasmi. Hivyo, mkakati huu unalenga kupima maeneo yote ya vizimba na kuweka alama za kudumu ili kujua idadi ya vizimba vyote, mahali vilipo na thamani yake.
Uboreshaji wa huduma ya maji Uwanjani.
Kwa muda mrefu sasa, uwanja wa Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki umekuwa ukikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji. Hali hii imekuwa ikiathiri utekelezaji wa shughuli za wadau ikiwemo upandaji wa vipando na hivyo kupunguza ufanisi wa shughuli zao. Kwa kauli moja, Kamati kuu imeazimia kuchimba kisima kirefu ambacho kitasaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji na hivyo kuongeza ufanisi wa huduma za wadau wa maonesho.
Uboreshaji wa huduma za Ulinzi na Usafi wa Mazingira.
Hatua hii inatokana na changamoto ya ukosefu wa huduma ya Ulinzi na Usafi katika Uwanja wa Nane Nane Kanda ya Mashariki. Hali hii imesababisha uwanja kuendelea kuwa mchafu na miundombinu ya uwanja kuharibiwa. Hivyo, Mpango Mkakati huu unapendekeza kuajiri watoa huduma ya Usafi wa mazingira na Ulinzi ili kuhakikisha kuwa miundombinu ya uwanja inalindwa na mazingira ya uwanja yanakuwa safi kwa mwaka mzima.
Uanzishwaji wa Kamati ya Usuruhishi wa Migogoro.
Kumeendelea kuwepo kwa migogoro ya umiliki wa ardhi ndani ya uwanja wa maonesho ambako kumechangiwa na udhaifu wa mfumo wa ugawaji na Usimamizi wa ardhi wakati wa TASO. Hivyo, Mpango mkakati unapendekeza kuanzishwa kwa Kamati ya Utatuzi wa Migogoro ili kuharakisha shughuli za maboresho ya Uwanja.
HITIMISHO.
Ili kufikia maono haya, Sekretarieti za Mikoa ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga zinaomba kupewa kibali cha muda mrefu (angalau miaka 20) ili ziweze kuratibu maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki. Hatua hii itawezeha kufanya maboresho makubwa ya uwanja wa Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki.