Kuhusu sisi

Historia ya Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki


Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki yalianza mwaka 1993 chini ya kilichokuwa Chama cha Wakulima Tanzania yaani “Tanzania Agricultural Society Organization” kwa kifupi TASO. Hata hivyo, kutokana na sababu za kiutendaji, kuanzia Mwaka 2017, Serikali iliisimamisha TASO kuendelea na uratibu wa maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki na jukumu hilo kukabidhiwa kwa Sekretarieti za Mikoa ya Kanda ya Mashariki inayojumuisha Mikoa minne (4) ya Dar es Salaam, Morogoro, Pwani na Tanga.

Lengo la Maonesho haya ni kuwakutanisha wadau mbalimbali ili kubadilishana uzoefu, kujifunza teknolojia mpya na upatikanaji wa masoko katika kuendeleza Kilimo, Ufugaji na Uvuvi.  Maonesho haya hufanyika katika Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuanzia tarehe 1 hadi tarehe 8 Agosti ya kila mwaka. 

Kupitia Maonesho haya, wananchi hupata mbinu mpya za kuongeza tija katika uzalishaji, usindikaji na kupata malighafi za kutosha kwa ajili ya Viwanda vyetu. Washiriki wa Maonesho ya Nane Nane wamegawanyika katika makundi mawili; kundi la kwanza ni la waoneshaji ambalo hujumuisha Wizara mbalimbali, Halmashauri za Wilaya, Mashirika ya Umma, Makampuni, Taasisi za fedha na Vyuo mbalimbali. Kundi la pili linajuisha wananchi wote wakiwemo Wakulima, Wafugaji, Wavuvi na Wajasiriamali. Kwa ujumla, makundi yote mawili hutegemeana, ambapo wanaotembelea maonesho huona teknolojia na bidha mpya na waoneshaji hupata wateja na kupata mrejesho juu ya huduma zao. Aidha, kwa kuwakutanisha Wakulima,Wafugaji, Wavuvi na watoa huduma mbalimbali kama wauza pembejeo na wanunuzi wa bidhaa imewawezesha wakulima kujenga mtandao mkubwa na kuongeza tija.

Tangu Sekretarieti za Mikoa zipewe Mamlaka ya kuratibu shughuli za usimamizi wa Uwanja wa Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki, kumekuwa na mafanikio mbalimbali kama inavyofafanuliwa kwenye muhtasari wa Mpango Mkakati wa Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki.