SAMAKI WA MAPAMBO NI FURSA
Rashid H Rashid ni kijana mjasiriliamali anaejishughulisha na uuzaji wa samaki wa mapambo na utengenezaji wa tanki za kuhifadhia samaki hao yajulikanayo kwa jina la “aquarium”
Rashid amepata fursa ya kushiriki maonesho ya nanenane yanayofanyika Mkoani Morogoro viwanja vya J. K Nyerere ndani ya Banda la Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.
Akiwa ndani ya Banda hilo amefanikiwa kutueleza masuala mbalimbali yanayohusu samaki wa mapambo ambapo amesema kuwa samaki wanaotumika kwa ajili ya mapambo ni wale wa maji baridi yaani wanaopatikana kwenye mito na maziwa na sio wa baharini “maji chumvi”
Ameendelea kueleza soko la samaki hao ni kubwa na linazidi kuongezeka kwani tafiti zinaonesha kuwa mauzo ya samaki hao duniani kote kwa mwaka 2021 yalifika Dola Bilioni 5.4, mwaka 2022 yalifika Dola Bilioni 5.8 na hapo yaliathiriwa na uwepo wa korona na kwa mwaka 2030 yanatarajiwa kufikia zaidi ya Dola Bilioni 11.
Aidha, Rashid ametoa wito kwa jamii kubadilisha dhana ya kuwa samaki ni kwa ajili ya chakula tu kitu ambacho si kweli kwani kuna samaki wa mapambo ambao wanaweza kutumika kama mapambo majumbani, maofisini na hata kwenye kumbi mbalimbali pia wanasaidia kuondoa mawazo kwa namna wanavyoonekana wakiwa kwenye aquarium
Sambamba na hayo Rashid amesema unaweza kutumia samaki hao kama fursa ya biashara kwani soko lipo lakini ijapokuwa sio maarufu na unaweza kuuza kwa watu mbalimbali na kwa sasa wanunuzi wengi wa samaki hao ni wazungu na wahindi.
Rashid anafuga na kuuza aina mbalimbali ya samaki wa mapambo akiwemo gold fish red cup, telescope, betta fish danio (zebra), mini pilot, guppy, Molly black and common, Molly gold and panda, guram, butterfly, paradise na wengine wengi wa aina hiyo na anayapata na elimu ya namna ya kuwatunza samaki hao.
Tembelea Banda la Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo uweze kujifunza bure fursa za kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na fursa za ujasiriamali kutoka kwa wajasiriamali wanapatikana ndani ya Banda hilo.