NJOONI MJIFUNZE KILIMO CHA MJINI
Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Dkt. Paul Kisaka, amewaalika watu wote wanaotembelea Uwanja wa Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Nane Nane, wa Mwl. J. K. Nyerere, uliopo katika Manispaa ya Morogoro, kufika katika Banda la Halmashauri ya Jiji la Tanga kuona na kujifunza kilimo na ufugaji wa mjini wenye tija unaowawezesha wakazi wa mjini kushiriki katika eneo dogo bila kuleta kero kwa wakazi wengine.
Dkt. Kisaka amesema Halmashauri ya Jiji la Tanga imejiandaa vya kutosha kwa ajili ya kutoa elimu inayohusiana na ufugaji, uvuvi na kilimo. Amesema katika Tanga Jiji, ambayo ni sehemu ya mjini, ufugaji wa ng'ombe unaotekelezwa ni wa ng'ombe wa maziwa ambao wanafugwa ndani.
Amesema katika maonesho haya, wataonyesha na kufundisha ufugaji mbalimbali ikiwemo ufugaji wa kuku, ufugaji wa mbuzi walioboreshwa, ufugaji wa samaki kwenye bwawa, bata bukini, na mengineyo.
"Lakini pia tunaonyesha ni namna gani ambavyo Halmashauri ya Jiji la Tanga imewawezesha vijana katika kujiendeleza kiuchumi, kujenga uchumi wa vijana, ufugaji wa kaa, kilimo cha mwani kwa wakina mama na vijana ambao wanalima katika pwani ya Bahari ya Hindi" Alisema Kisaka.
Akizungumzia kilimo cha mjini, Daktari Kisaka amesema ni kilimo kinachochukua nafasi ndogo cha mazao ya bustani, mbogamboga, ambacho huweza kufanyika hata kwa wanaoishi ghorofani.
Halmashauri ya Jiji la Tanga ni moja kati ya Majiji mawili yaliyopo kanda ya Mashariki ya Maonesho hayo, Jiji jingine likiwa ni la Dar es Salaam.
Sherehe za Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nane Nane) Kanda ya Mashariki zimefunguliwa rasmi Augosti 01, 2023 na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda, na zitahitimishwa tarehe 8 Agosti, 2023.
Posted in Tangazo on Aug 03, 2023